TANGAZO LA KAZI ZA MUDA ZA MAKARANI NA WASIMAMIZI WA SENSA 2022.

Location:
Date Posted: May 6, 2022
Application deadline: May 19, 2022

UTANGULIZI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iko kwenye maandalizi ya kufanya Sensa ya Watu na Makazi ambayo itafanyika tarehe 23 Agosti 2022. Ili kufanikisha Sensa hii, Serikali inatangaza nafasi za kazi za muda za MAKARANI NA WASIMAMIZI WA SENSA kwa Watanzania wenye nia na sifa zinazostahili kama ilivyoainishwa katika tangazo hili.

1. KARANI WA SENSA

a) Kazi za Kufanya

Mwombaji wa nafasi hii, endapo atachaguliwa atatakiwa kuhudhuria mafunzo ya makarani ambapo baada ya mafunzo ikiwa atafaulu atatakiwa kurejea katika eneo alilotokea au kupangiwa eneo lingine lolote kwa ajili ya kutekeleza kazi zifuatazo:-

i) Kutambua mipaka ya eneo la kuhesabia watu kwa kulinganisha na ramani ya eneo la kuhesabia watu na maelezo ya mipaka yaliyopo kwenye ramani hiyo;

ii) Kushirikiana na msimamizi na uongozi wa eneo husika kutambua kama katika eneo la kuhesabia watu kuna makundi maalaum yanayotakiwa kuhesabiwa kwa utaratibu maalum tofauti na kaya za kawaida;

iii) Kuhoji dodoso la jamii katika ngazi ya kitongoji/mtaa/shehia;

iv) Kuhesabu watu wote waliolala ndani ya mipaka ya eneo la kuhesabia watu usiku wa kuamkia siku ya Sensa ndani ya muda uliopangwa;

v) Kutuma katika mfumo kazi zilizofanyika na kukamilika kila siku Makao Makuu ya NBS/OCGS;

vi) Kuvitumia vifaa vyote na nyaraka za Sensa kwa kadiri ya malengo yaliyokusudiwa; kuvitunza na kuviwasilisha kwa Msimamizi baada ya kazi kukamilika;

vii) Kutoa taarifa kwa Msimamizi wa Sensa kuhusu changamoto za utekelezaji wa majukumu ya kuhesabu watu;

viii) Kuhesabu majengo yote katika eneo husika ndani ya muda uliopangwa;

ix) Kusajili anwani zote za makazi katika eneo husika ndani ya muda uliopangwa na;

x) Kufanya kazi nyingine zinazohusiana na Sensa atakazopangiwa na Kiongozi wake.

b) Sifa za Mwombaji

Mwombaji wa nafasi hii anatakiwa awe na sifa zifuatazo:-

i) Awe na umri kati ya miaka 18 hadi 45 na mwenye afya njema;

ii) Awe na elimu ya kidato cha nne au zaidi;

iii) Awe ni mtumishi wa umma au sekta binafsi au yeyote asiye na ajira anayeishi katika eneo husika;

iv) Awe na uzoefu wa kutumia simu janja/ kishikwambi;

v) Asiwe amewahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai; na

vi) Kuwa na taaluma ya takwimu, hisabati, mipango, uchumi, au cheti cha ukusanyaji wa takwimu rasmi au uzoefu wa kufanya kazi za kitakwimu ni sifa ya ziada.

2. MSIMAMIZI WA SENSA

2.1 MSIMAMIZI WA MAUDHUI (CONTENT SUPERVISOR)

a) Kazi za Kufanya

Mwombaji wa nafasi hii, endapo atachaguliwa atatakiwa kuhudhuria mafunzo ya Wasimamizi wa Sensa ambapo baada ya mafunzo ikiwa atafaulu atatakiwa kuhudhuria mafunzo ya makarani wa Sensa kisha kurejea katika eneo alilotokea au kupangiwa eneo lingine lolote kwa ajili ya kutekeleza kazi zifuatazo:-

i) Kuhakikisha kuwa kila karani wa Sensa anatambua eneo la kuhesabia watu;

ii) Kuhakikisha kwamba kila karani ana vifaa muhimu kama ilivyoorodheshwa katika "Mwongozo wa Karani wa Sensa".

iii) Kuhakikisha kuwa makarani wameelewa kazi na ratiba zao zimeandaliwa vizuri na wanazifuata;

iv) Kuhakikisha kuwa dodoso la jamii katika ngazi ya Kitongoji/Mtaa/Shehia limehojiwa kikamilifu na karani husika ndani ya siku tatu kabla ya siku ya kuhesabu watu;

v) Kushirikiana na uongozi wa eneo husika kutambua kama katika eneo la kuhesabia watu kuna makundi maalaum yanayotakiwa kuhesabiwa kwa utaratibu maalum tofauti na kaya za kawaida;

vi) Kugawa kaya kwa kila karani kulingana na utaratibu uliopangwa iwapo eneo moja la kuhesabia watu litakuwa na karani zaidi ya mmoja na kuhakikisha kaya zote katika eneo husika zinahesabiwa na zinahesabiwa mara moja tu;

vii) Kuhakikisha kuwa watu wote waliolala ndani ya mipaka ya eneo la kuhesabia watu usiku wa kuamkia siku ya Sensa wamehesabiwa;

viii) Kuhakikisha kuwa kila jengo katika Kitongoji/Eneo la kuhesabia limefikiwa na kuhesabiwa baada ya zoezi kuu la Sensa kwa kuzingatia maeneo ambayo Karani wa Sensa aligawiwa wakati wa zoezi la kuhesabu watu;

ix) Kuhakikisha kuwa anwani zote za makazi katika Kitongoji/Eneo la kuhesabia zimesajiliwa;

x) Kuhakikisha kuwa anafanya mawasiliano na makarani mara kwa mara, na kutathmini utendaji wao wa kazi na inapobidi, atoe mwongozo wa ziada;

xi) Kushauriana na viongozi mbalimbali na mamlaka za juu ikiwa kuna changamoto ambazo zinahitaji maamuzi ya ngazi hiyo;

xii) Kukagua na kuhakikisha karani wa Sensa ametuma kazi yake makao makuu ya NBS/OCGS kulingana na utaratibu uliowekwa;

xiii) Kutumia fomu mbalimbali za udhibiti wa vifaa na mwenendo wa zoezi la Sensa kwa ujumla; na

xiv) Kufanya kazi nyingine zinazohusiana na Sensa atakazopangiwa na Kiongozi wake.

b) Sifa za Mwombaji

Mwombaji wa nafasi hii anatakiwa awe na sifa zifuatazo:-

i) Awe na umri wa miaka 18 au zaidi na mwenye afya njema;

ii) Awe na elimu ya kidato cha nne au zaidi;

iii) Awe ni mtumishi wa umma au sekta binafsi au yeyote asiye na ajira anayeishi katika eneo husika;

iv) Awe na uzoefu wa kutumia simu janja/ kishikwambi;

v) Asiwe amewahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai; na

vi) Kuwa na taaluma ya takwimu, hisabati, mipango, uchumi au uzoefu wa kusimamia kazi za kitakwimu ni sifa ya ziada.

2.2 MSIMAMIZI WA TEHAMA (IT SUPERVISOR)

a) Kazi za Kufanya

Mwombaji wa nafasi hii, endapo atachaguliwa atatakiwa kuhudhuria mafunzo ya Wasimamizi wa Sensa ambapo baada ya mafunzo ikiwa atafaulu atatakiwa kuhudhuria mafunzo ya makarani wa Sensa kisha kurejea katika eneo alilotokea au kupangiwa eneo lingine lolote kwa ajili ya kutekeleza kazi zifuatazo:-

i) Kuhakikisha kwamba kila karani ana kishikwambi chenye mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Mfumo wa Ukusanyaji wa Taarifa za Anwani za Makazi kinafanya kazi kwa ufanisi;

ii) Kuhakikisha kuwa kila karani ana power bank, charger pamoja na vifaa vingine vya TEHAMA kama ilivyoorodheshwa katika "Mwongozo wa Karani wa Sensa" na vinafanya kazi kwa ufanisi;

iii) Kuhakikisha kuwa anafanya mawasiliano na makarani mara kwa mara kuhusu masuala ya TEHAMA, na kutathmini utendaji wao wa kazi wa kutumia vishikwambi na inapobidi, atoe mwongozo wa ziada;

iv) Kutatua changamoto zote za TEHAMA ambazo zinaweza kutokea wakati wa zoezi la kuhesabu watu, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi;

v) Kutoa msaada wa kitaalamu ili kuhakikisha kuwa karani wa Sensa anatuma kazi iliyokamilika makao makuu kwa wakati na kuhakikisha kuwa kazi hiyo imepokelewa; na

vi) Kufanya kazi nyingine za TEHAMA zinazohusiana na Sensa atakazopangiwa na Kiongozi wake.

b) Sifa za Mwombaji

Mwombaji wa nafasi hii anatakiwa awe na sifa zifuatazo:-

i) Awe na umri kati ya miaka 18 hadi 45 na mwenye afya njema;

ii) Awe na elimu ya kidato cha nne au zaidi;

iii) Awe na elimu ya TEHAMA angalau ngazi ya stashahada (Diploma);

iv) Awe ni mtumishi wa umma au sekta binafsi au yeyote asiye na ajira anayeishi katika eneo husika;

v) Awe na uzoefu wa kutumia simu janja/ kishikwambi;

vi) Asiwe amewahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai; na

vii) Kuwa na uzoefu wa kazi za kitakwimu zinazotumia teknolojia ya kielekroniki ni sifa ya ziada.

3. NAMNA YA KUTUMA MAOMBI

Mtanzania mwenye sifa zilizotajwa hapo juu atume maombi yake kwa njia ya mtandao kupitia www.pmo.go.tz; www.tamisemi.go.tz au www.nbs.go.tz kwa waombaji kazi wa Tanzania Bara na www.ompr.go.tz; https://www.tamisemim.go.tz au www.ocgs.go.tz kwa waombaji kazi wa Tanzania Zanzibar. Waombaji wanashauriwa kufuata maelekezo yote yaliyotolewa katika tovuti hizi kuhusiana na ajira hizi. Maombi haya ya ajira hayalipiwi.

Maombi hayo yatumwe kwa kujaza fomu iliyopo katika mtandao ambayo ikikamilika kujazwa, na kwa kufuata maelekezo kwa kadiri anavyojaza hatua kwa hatua, mwombaji kazi atafika hatua inayomhitaji kupakua Fomu ya Sensa Na.1 ya maombi ya kazi ambayo baada ya kuipakua atatakiwa kui-print na kukamilisha sehemu za wadhamini, kiongozi wa serikali ya mtaa/shehia/kijiji, pamoja na kusainiwa na mwombaji.

Baada ya kukamilisha ujazaji katika maeneo hayo mwombaji atatakiwa kui-scan katika mfumo wa PDF na kurejea katika mtandao wakati wowote ndani ya siku zilizotolewa, na kuipakia mtandaoni na kukamilisha mchakato wa maombi ya kazi.

Muhimu:

Nakala au kivuli (copy) ya fomu iliyojazwa kikamilifu ipelekwe katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata/Sheha/Mtaa/Kijiji anakotakiwa kufanyia kazi mwombaji kwa ajili ya rejea wakati wa uchambuzi. Maombi yote yawasilishwe kuanzia tarehe 05 hadi 19 Mei 2022.

“SENSA KWA MAENDELEO, JIANDAE KUHESABIWA”


Download